Chaji ya umeme
Chaji ya umeme ni tabia ya mata na kila kitu huwa na chaji aina mbili ndani yake. Chaji hizi mbili ni kinyume zinaitwa chaji hasi na chaji chanya. Mara nyingi chaji haionekani kwa sababu hizi aina mbili za chaji zinajibatilishana. Lakini kama idadi ya elektroni ndani ya kitu ina upungufu au ziada kulingana na hali ya kawaida tunaona kitu hiki kina chaji, ama chanya au hasi.
Chaji umeme na muundo wa atomu
[hariri | hariri chanzo]Kila kitu hujengwa kwa atomu na kila atomu ina chembe ndogo zaidi ndani yake. Kati ya chembe ndogo ndani ya atomu kuna elektroni na protoni zilizo na chaji mbili za kinyume ilhali elektroni huitwa "hasi" na protoni huitwa "chanya". Kila chembe huwa na kizio kimoja cha chaji, ama hasi au chanya. Kwa kawaida kila atomu huwa na idadi ileile ya protoni na elektroni hivi chaji zao zinajibatilishana katika atomu na atomu kwa jumla haionyeshi chaji.
Protoni (pamoja na neutroni zisizo na chaji) zinafanya kiini cha atomu na zinabaki mahali pao. Lakini elektroni zinazunguka kiini katika mzingo elektroni na hapa inatokea ya kwamba elektroni inahamia atomu nyingine. Kama elektroni inatoka katika atomu yake ya asili na kuhamia nyingine uwiano sawa baina ya elektroni na protoni katika atomu husika haipo tena.
Pale ambako elektroni imetoka kuna protoni zaidi kuliko elektroni na hapa tunasema atomu hii ina chaji chanya. Kinyume katika atomu iliyopokea elektroni kutoka nje kuna ziada ya elektroni juu ya idadi ya protoni na hapa tunasema atomu imekuwa na chaji hasi.
Kutokea kwa chaji hasi au chanya
[hariri | hariri chanzo]Kutokea kwa chaji hasi au chanya katika gimba fulani ni kwa sababu chaji zilizokaa pamoja kabla zimetenganishwa. Njia inayotokea kila siku ni kwa msuguano. Kwa kusugua kipande cha plastiki (au: kioo) na sufi kunatokea chaji. Kwa mfano kusugua mipira miwili kwenye sufi ya sweta kunaweka chaji kwa yote miwili. Tukiishika kwa kamba na kupeleka karibu haitaki kugusana. Maana chaji hasi pande zote mbili zinapigana. Lakini tukishika mpira uliosuguliwa juu ya vipande vidogo vya karatasi hizi zitavutwa na mpira jinsi msumali anavutwa na sumaku. Radi wakati wa ngurumo ni tokeo la chaji zinazotokea hewani kutokana na msuguano wa hewa.
Njia nyingine ya kujenga chaji inayotumiwa kwa teknolojia ni kwa kemia yaani kwa kuchangaya dutu na viowevu zinazoanzisha mchakato wa kikemia unaosababisha kutokea kwa ioni na hivyo chaji.