Nenda kwa yaliyomo

Jumapili ya matawi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Padri Mkatoliki akibariki matawi huko Plaridel, Bulacan, Ufilipino.
Baraka ya mitende nje ya kanisa la Anglikana huko Marekani.
Mwaka wa liturujia
Magharibi
Mashariki

Jumapili ya matawi (pia: Jumapili ya mitende) katika mwaka wa Kanisa wa madhehebu mbalimbali ya Ukristo ndiyo siku inapoadhimishwa jinsi Yesu Kristo alivyoingia mara ya mwisho Yerusalemu ili kufa na kufufuka kwa wokovu wa binadamu wote.

Kadiri ya Injili zote[1], siku hiyo alishangiliwa na umati mkubwa, hasa wa vijana, kwa kutumia matawi, ndiyo asili ya jina. Kufuatana na habari hiyo, mara nyingi Wakristo wanafanya maandamano ya ibada wakiimba na kupunga matawi, mara nyingi ya mitende inapopatikana, kulingana na taarifa iliyomo katika Injili ya Yohane.

Jumapili hiyo ndiyo mwanzo wa Juma kuu linaloadhimisha matukio makuu ya historia ya wokovu kadiri ya imani ya Wakristo.

Tangu mwaka 1985, kwa uamuzi wa Papa Yohane Paulo II, katika siku hiyo Kanisa Katoliki linaadhimisha pia "Siku ya kimataifa ya vijana", kwa sababu, kadiri ya Injili, watu wa rika hilo ndio waliomshangilia zaidi Yesu akiingia Yerusalemu.

Jumapili ya matawi ikiadhimishwa na Waorthodoksi wa Biškek huko Kirgizistan.

Habari ilivyo katika kila Injili

[hariri | hariri chanzo]

11:1 Walipokuwa wanakaribia Yerusalemu walifika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni. Hapo aliwatuma wawili wa wanafunzi wake, 2 akawaambia, "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia humo, mtakuta mwana punda amefungwa ambaye bado hajatumiwa na mtu. Mfungueni mkamlete. 3 Kama mtu akiwauliza, `Mbona mnafanya hivyo?` Mwambieni, `Bwana anamhitaji na atamrudisha hapa mara."` 4 Basi, wakaenda, wakamkuta mwana punda barabarani amefungwa mlangoni. Walipokuwa wakimfungua, 5 baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo wakawauliza "Kwa nini mnamfungua huyo mwana punda?" 6 Wanafunzi wakajibu kama Yesu alivyokuwa amewaambia; nao wakawaacha waende zao. 7 Wakampelekea Yesu huyo mwana punda. Wakatandika mavazi yao juu ya huyo mwana punda, na Yesu akaketi juu yake. 8 Watu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani; wengine wakatandaza matawi ya miti waliyoyakata mashambani. 9 Watu wote waliotangulia na wale waliofuata wakapaaza sauti zao wakisema, "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! 10 Ubarikiwe Ufalme ujao wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni!" 11 Yesu aliingia mjini Yerusalemu akaenda moja kwa moja mpaka Hekaluni, akatazama kila kitu kwa makini. Lakini kwa vile ilikwisha kuwa jioni, akaenda Bethania pamoja na wale kumi na wawili.

21:1 Yesu na wanafunzi wake walipokaribia Yerusalemu na kufika Bethfage katika mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, 2 akawaambia, "Nendeni hadi kijiji kilicho mbele yenu na mtamkuta punda amefungwa na mtoto wake. Wafungueni mkawalete kwangu. 3 Kama mtu akiwauliza sababu, mwambieni, `Bwana anawahitaji,` naye atawaachieni mara." 4 Jambo hili lilifanyika ili yale yaliyosemwa na nabii yatimie: 5 "Uambieni mji wa Sioni: Tazama, Mfalme wako anakujia! Ni mpole na amepanda punda, mwana punda, mtoto wa punda." 6 Hivyo, wale wanafunzi walienda wakafanya kama Yesu alivyowaagiza. 7 Wakamleta yule punda na mtoto wake, wakatandika nguo zao juu yao na Yesu akaketi juu yake. 8 Umati mkubwa wa watu ukatandaza nguo zao barabarani, na watu wengine wakakata matawi ya miti wakayatandaza barabarani. 9 Makundi ya watu waliomtangulia na wale waliomfuata wakapaaza sauti: "Hosana Mwana wa Daudi! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana! Hosana Mungu juu mbinguni!"

10 Yesu alipokuwa anaingia Yerusalemu, mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawa wanauliza, "Huyu ni nani?" 11 Watu katika ule umati wakasema, "Huyu ni nabii Yesu, kutoka Nazareti katika mkoa wa Galilaya." 12 Basi, Yesu akaingia Hekaluni, akawafukuza nje watu waliokuwa wanauza na kununua vitu ndani ya Hekalu; akazipindua meza za wale waliokuwa wanavunja fedha, na viti vya wale waliokuwa wanauza njiwa. 13 Akawaambia, "Imeandikwa katika Maandiko Matakatifu: `Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala.` Lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi." 14 Vipofu na vilema walimwendea huko Hekaluni, naye Yesu akawaponya. 15 Basi, makuhani wakuu na walimu wa Sheria walipoyaona maajabu aliyoyafanya Yesu, na pia watoto walipokuwa wanapaaza sauti zao Hekaluni wakisema: "Sifa kwa Mwana wa Daudi," wakakasirika. 16 Hivyo wakamwambia, "Je, husikii wanachosema?" Yesu akawajibu, "Naam, nasikia! Je hamjasoma Maandiko haya Matakatifu? `Kwa vinywa vya watoto wadogo na wanyonyao unajipatia sifa kamilifu."` 17 Basi, akawaacha, akatoka nje ya mji na kwenda Bethania, akalala huko.

19:28 Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu. 29 Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili, 30 akawaambia: "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana punda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungeni, mkamlete hapa. 31 Kama mtu akiwauliza, kwa nini mnamfungua, mwambieni, `Bwana ana haja naye."` 32 Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia. 33 Walipokuwa wanamfungua yule mwana punda, wenyewe wakawauliza, "Kwa nini mnamfungua mwana punda huyu?" 34 Nao wakawajibu, "Bwana anamhitaji." 35 Basi, wakampelekea Yesu yule mwana punda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake wakampandisha Yesu. 36 Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani. 37 Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake, wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona; 38 wakawa wanasema: "Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!"

39 Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu, wakamwambia Yesu, "Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!" 40 Yesu akawajibu, "Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti." 41 Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia 42 akisema: "Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako. 43 Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote. 44 Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa." 45 Kisha, Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuzia nje wafanyabiashara 46 akisema, "Imeandikwa: `Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala`; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang`anyi." 47 Yesu akawa anafundisha kila siku Hekaluni. Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza, 48 lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.

12:12 Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu. 13 Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaaza sauti wakisema: "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli." 14 Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko: 15 "Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana punda." 16 Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo. 17 Kundi la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia. 18 Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo. 19 Basi, Mafarisayo wakaambiana, "Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata."

  1. Mk 11:1–11, Math 21:1–17, Lk 19:28–48, Yoh 12:12–19

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Wikimedia Commons ina media kuhusu:
Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Jumapili ya matawi kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.