Kasi ya nuru (pia: kasi ya mwanga, kwa Kiingereza speed of light) ni kasi yake iliyopimwa hata imekubaliwa kuwa nuru inakwenda karibu kilomita laki tatu kwa sekunde moja [1] katika ombwe. Kama nuru inapitia katika hewa kasi yake inapungua.

Mwanga wa jua unachukua takribani dakika 8 na sekunde 17 kusafiri umbali wa wastani kutoka kwenye uso wa Jua hadi Duniani

Katika nadharia ya uhusianifu ya Albert Einstein kasi ya nuru inadhaniwa kuwa ileile wakati wowote, pia katika hali yoyote. Yaani kasi inabaki ileile hata kama nuru inatoka katika chombo chenye kasi yenyewe au kama mtazamaji ana mwendo wake mwenyewe. Katika nadharia hiyo hakuna mwendo wenye kasi kushinda nuru. Kasi ya nuru imekuwa kipimo cha msingi katika sayansi za fizikia na unajimu.

Kasi hiyo haihusu nuru pekee inayoonekana na macho ya binadamu lakini pia kwa aina mbalimbali ya mnururisho kama mawimbi ya redio n.k.

Tangu safari ya kwanza ya watu kufika juu ya mwezi chini ya Mradi wa Apollo wa NASA tabia ya nuru kuwa na kasi ilionekana kwa watazamaji wote. Kila safari kituo cha NASA katika mji wa Houston iliwaita wanaanga kwa redio: jibu lilichukua sekunde kadhaa hadi kufika kutokana na umbali wa kilomita lakhi tatu kati ya dunia na mwezi, hivyo mazungumzo yaliendelea kwa vituo vya kusubiri hadi sauti ilipofika na kurudi.

Kama siku moja wanaanga watasafiri mbali zaidi, hadi Mirihi au Zohali ,muda huu utaongezeka kutokana na umbali na kasi ya nuru inayobaki ileile.

Tanbihi

hariri
  1. Kikamilifu ni mita 299,792,458 kwa sekunde moja