Johann Bayer (15727 Machi 1625) alikuwa mwanasheria na mwanaastronomia kutoka nchi ya Ujerumani. Alianzisha mfumo unaotumika hadi leo wa kutaja mahali pa nyota angani kufuatana na kundinyota na mwangaza unaoonekana. Majina ya Bayer hutumiwa kwa nyota angavu zinazoonekana vema kwa macho matupu.

Kundinyota la Orion (Jabari) katika Uranometria ya Johann Bayer

Maisha

Alizaliwa mwaka 1572 mjini Rain katika Bavaria.

Alipokuwa na miaka 20 alianza masomo yake ya falsafa na sheria katika chuo kikuu cha Ingolstadt.

Baada ya kumaliza masomo yake alihamia Augsburg alipofanya kazi ya mwanasheria akawa mshauri wa kisheria wa halmashauri ya mji kuanzia mwaka 1612.[1]

Nje ya kazi yake alijisomea elimu katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na akiolojia, hisabati na astronomia.

Hakuunda familia yake, bali alibaki kapera bila kuoa akafa mwaka 1625.

Kazi

Bayer amekuwa maarufu kwa atlasi yake ya nyota ya Uranometria ("Uranometria Omnium Asterismorum" - "Ramani ya anga ya makundinyota yote") iliyochapishwa mara ya kwanza mjini Augsburg mwaka 1603.

Hii ilikuwa ramani ya nyota ya kwanza iliyoonyesha pia nyota zinazoonekana tu kwenye angakusi ya Dunia, kazi iliyowezeshwa na safari za upelelezi tangu meli za Ferdinand Magellan kuzunguka Dunia yote mara ya kwanza mwaka 1521. [2] 

Hii ilikuwa atlasi ya kwanza ya nyota yenye ramani 51: moja-moja kwa ajili ya kila kundinyota lilojulikana tangu zamani za Ptolemaio ukurasa unaoonyesha kundinyota mpya kwenye nusutufe ya kusini zilizobuniwa na Petrus Plancius na ramani mbili za angakusi na angakaskazi. Kila ramani ina alama za kuonyesha longitudo na latitudo alizochukua kutoka orodha ya nyota ya Tycho Brahe ambayo haikuchapishwa bado wakati wa kutolewa kwa Uranometria.

Bayer alitumia kazi ya Tycho Brahe, inawezekana alitumia pia atlasi ya nyota ya Alessandro Piccolomini ya mwaka 1540 ingawa Bayer aliongeza zaidi ya nyota 1,000 kwa orodha za watangulizi wake.

Katika kitabu cha Uranometria alianzisha mfumo mpya wa kutaja nyota inayojulikana kama "majina ya Bayer". Humo alipanga kila nyota katika kundinyota fulani. Ndani ya kundinyota aliipa kila nyota herufi ya Kigiriki kufuatana na uangavu: nyota angavu zaidi iliitwa Alfa, iliyofuata Beta, halafu Gamma na kadhalika.

Katika atlasi yake aliingiza makundinyota 12 mpya zilizobuniwa miaka michache iliyopita kutaja nyota za angakusi ambazo hazikujulikana na wataalamu wa Ugiriki ya Kale na Roma ya Kale.[3]

Heshima baada ya kufa

Kwenye Mwezi wa Dunia kuna kasoko iliyopokea jina la Bayer kwa heshima yake.

Tazama pia

Marejeo

  1. Hockey, Thomas (2009). The Biographical Encyclopedia of Astronomers. Springer Publishing. ISBN 978-0-387-31022-0. Iliwekwa mnamo Agosti 22, 2012.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. Ridpath, Ian. "Johann Bayer's southern star chart".
  3. Kanas, Nick (2009). Star Maps: History, Artistry, and Cartography (tol. la 2nd). Springer. uk. 119-120. ISBN 978-1-4614-0916-8.