Kitabu cha Ezekieli

(Elekezwa kutoka Ezekieli)

Kitabu cha Ezekieli kinamhusu mmojawapo kati ya manabii muhimu zaidi wa Agano la Kale, Ezekieli, aliyefanya kazi ya unabii miaka 592-570 hivi K.K., kadiri ya ushahidi wa kitabu chake.

Moja ya njozi 4 za Ezekieli.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Mazingira

hariri

Baada ya maangamizi ya Yerusalemu, polepole Wayahudi waliohamishiwa Babeli waliweza kujitafutia kazi (kwanza kilimo, halafu biashara), wakafaulu sana, hata wengine wakawa watumishi wa serikali.

Lakini upande wa dini walikuwa hatarini, kwa sababu imani ya Mwisraeli inategemea taifa, nchi na hekalu ambavyo vyote vilikuwa vimeharibika.

Kwa ajili yao Mungu akatuma tena manabii, hasa Ezekieli ambaye anaonekana kuwa alihamishwa mapema tangu mwaka 598 K.K. pamoja na viongozi wengine 8,000 hivi.

Habari zake tunazipata katika kitabu chake tu, anapotajwa kwa jina mara tatu, kumbe kwa kawaida Mungu anamuita “binadamu”. Kabla hajahamishwa aliweza kumfahamu nabii Yeremia, na kweli aliathiriwa na ujumbe wake ambao aliuunga mkono na kuuendeleza.

Kazi ya Ezekieli

hariri

Alifanya unabii wake hukohuko uhamishoni, ingawa ujumbe wake uliwalenga waliobaki Yuda pia. Kwanza aliwatolea maneno ya hukumu ili watubu kabla hawajaangamia, lakini baadaye akawapa maneno ya faraja wasikate tamaa. Katika kuwahakikishia kuwa wataanza upya nchini kwao aliwapa maelekezo yote kwa ajili hiyo. Kwa namna ya pekee, akiwa kuhani, kama vile Yeremia, katika kitabu chake alishughulika sana na hekalu na mambo ya ibada.

Upande mwingine alianzisha mtindo mpya wa unabii ambao unaitwa wa Kiapokaliptiko (kilele chake ni Ufunuo wa Yohane) na ambao hauhusu tena matukio madogomadogo ya sasa, bali kwa njozi za ajabuajabu unaonyesha maana ya historia yote mpaka mwisho. Njozi 4 anazozisimulia kinaganaga na zisizosahaulika (utukufu wa Mungu kuhama hekalu, utukufu huo kurudi hekaluni, hekalu kutokwa na maji yenye uwezo wa kuponya hata Bahari ya Kifo, hatimaye mifupa mikavu kusimama na kuishi tena) zinachukua nafasi kubwa katika kitabu chake na kwa mafumbo yake yanavutia ubunifu wetu ujitahidi kuelewa yaliyofichika katika mifano, tarakimu, rangi n.k.

Dini ya Kiyahudi mpaka leo inategemea sana kazi aliyoifanya Ezekieli ya kukazia utekelezaji wa Torati hata pasipo uhuru wa kisiasa. Muhimu kwake ni kwamba Wayahudi popote walipo wamtukuze Mwenyezi Mungu kwa kufuata sheria yake. Tena alitabiri kuwa Mungu tu atawawezesha kufanya hivyo kwa kugeuza mioyo yao migumu kama mawe yadunde kama ile ya nyama, au vizuri zaidi kwa kuwatia moyo mpya na roho mpya wazishike amri zake (11:17-20; 36:26). Mungu atawaokoa kabla hawajatubu ili jina lake litukuzwe katika watu wake: wokovu anaouleta hautegemei matendo mema ya binadamu, bali muungano wa Mungu na wale walioitwa kwa jina lake (16:58-63). Hakuna kitabu kinachosisitiza utukufu wa Mungu kuliko hicho.

Vitabu vya Agano la Kale

Mwanzo * Kutoka * Walawi * Hesabu * Kumbukumbu * Yoshua * Waamuzi * Ruthu * Samueli I * Samueli II * Wafalme I * Wafalme II * Mambo ya Nyakati I * Mambo ya Nyakati II * Ezra * Nehemia * TobitiDK * YudithiDK * Esta * Wamakabayo IDK * Wamakabayo IIDK * Yobu * Zaburi * Methali * Mhubiri * Hekima DK * SiraDK * Wimbo Bora * Isaya * Yeremia * Maombolezo * BarukuDK * Ezekieli * Danieli * Hosea * Yoeli * Amosi * Obadia * Yona * Mika * Nahumu * Habakuki * Sefania * Hagai * Zekaria * Malaki

Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.

  Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kitabu cha Ezekieli kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.