Rijili Kantori
Rijili Kantori , Rijili Kantarusi au ing. Alpha Centauri (pia: Toliman au Rigil Kentaurus) ni nyota inayong'aa sana katika anga ya kusini kwenye kundinyota la Kantarusi (pia: ing. Centaurus). Ni nyota angavu ya nne angani lakini haionekani kwenye nusu ya kaskazini ya Dunia.
Kundinyota | Kantarusi (Centaurus) |
Mwangaza unaonekana | +1.33 |
Kundi la spektra | G2 V |
Paralaksi (mas) | 754.81 ± 4.11 |
Umbali (miakanuru) | 4.37 |
Mwangaza halisi | 5.71 |
Masi M☉ | 1.1 |
Nusukipenyo R☉ | 1.22 |
Mng’aro L☉ | 1.5 |
Jotoridi usoni wa nyota (K) | 5790 |
Muda wa mzunguko | siku 41 |
Majina mbadala | α Centauri, Toliman, Bungula, Gliese 559, FK5 538, CD−60°5483, CCDM J14396-6050, GC 19728 |
Alpha Centauri ni nyota ya pekee kwa sababu ni nyota yetu jirani katika anga ina umbali wa miakanuru 4.2. Inaonekana angani karibu na kundinyota la Salibu (Crux).
Jina
haririJina la Kiswahili ni Rijili Kantori[1] linalotokana na ar. رجل القنطور rijil-al-qantur. Maana ya jina ni "mguu wa kantori (kentauro)" maana mataifa ya kale waliona kundinyota lote kama picha ya kiumbe ambacho ni nusu farasi na nusu binadamu kulingana na mitholojia ya Kigiriki. Jina la kimagharibi "Rigel/Rigil Centauri"[1] linatokana na jina lilelile la Kiarabu kwa "mguu" yaani رجل inayoandikwa kwa herufi za Kilatini ama "rijil" au "rigil" au "rigel". Ilhali kuna nyota kadhaa zilizotazamiwa kama "mguu" kwenye picha za makundinyota, ni kawaida kuongeza jina la kundinyota yake.
Jina la kitaalamu kufuatana na mfumo wa Bayer ni Alfa Centauri kwa maana ya kwamba ilitazamiwa kuwa nyota ya kwanza katika uangavu kati ya nyota za Kantarusi (Centaur).
Mfumo wa nyota tatu
haririRijili Kantori (Alpha Centauri) inaonekana kama nyota moja lakini kwa darubini kubwa inaonekana kuwa mfumo wa nyota tatu zinazokaa karibu na kushikamana kati yao. Nyota mapacha za Alpha Centauri A na Alpha Centauri B ziko miakanuru 4.36 kutoka kwetu na nyota ya tatu Alpha Centauri C au Proxima Centauri ina umbali wa miakanuru 4.22.
Proxima Centauri (yaani nyota ya Kantarusi iliyo karibu zaidi nasi) imegunduliwa kuwa na sayari moja. Vipimo vinavyopatikana hadi sasa zinaonyesha uwezekano mkubwa ya kwamba sayari hii ni ya mwamba (kama dunia yetu, Mirihi au Zuhura) na inaweza kuwa na angahewa, tena katika upeo wa joto unaoruhusu kuwepo kwa uhai. [2]
Marejeo
hariri- ↑ Rijili Kantori ni umbo lililorekodiwa na Knappert (1993): "The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations." In: Indian Ocean Review, The. Perth, Australia, v, 6 n. 3, September 1993, uk 5-7
- ↑ Scientists take first tentative steps to explore potential climate of Proxima B, tovuti ya phys.org ya May 16, 2017